Zahera pakacha lako limejaa lakini .....? - Mase Kaleby

Breaking

Home Top Ad

Monday, 17 December 2018

Zahera pakacha lako limejaa lakini .....?


Shkamoo Zahera. Shkamoo papa musema kweli mutu ya Congo. Ni mmoja kati ya makocha wanaofanya vizuri sana ligi kuu Tanzania bara. Wengi wamekuwa wamimsema vibaya kuwa amekuwa msemaji wa timu. Wanaomteta Zahera kwa kejeli hizo tungependa watueleze msemaji wa Man U, au Barca au Madrid ni nani?

Msemaji mkuu wa timu ni kocha hawa wengine wanaopewa vyeo waongelee timu wakati hata mpira wa makaratasi hawakucheza ni siasa uchwara kwenye soka. Zahera anaiongoza Yanga kwa weledi mkubwa. Yeye ndiye anayepaswa kuiongelea timu yake na sio mtu mwingine. Zahera jina lake la pili ni Mwinyi. Weka nukta hapa

Jina moja maarufu sana hapa Tanzania. Nadhani mnamkumbuka mzee Mwinyi. Moja ya maraisi walionesha uthubutu mkubwa sana katika suala zima la uchumi na hasa hasa uwekezaji. Wengi walimpachika jina la Mzee Ruksa. Sitaki sana kwenda huko. Tubakie hapa hapa kwenye soka.

Zahera amesema RUKSA Beno kuondoka. Ni taarifa ya kushtua kidogo. Naona kama RUHUSA hii ya Kakolanya kwenda nayo imetoa RUHUSA kwa timu ya Yanga kuruhusu mabao mengi sana.

Katika magoli 11 waliyoruhusu msimu mzima, magoli 7 yamepatikana mechi 7 za mwisho ambazo Beno hakuwepo. Ikumbukwe katika mabao 4 yaliyobakia 3 yalifungwa Mh Klaus Kindoki akiwa golini wakati Kitenge akimchungulia kwa Hat trick.

Lakini cha kustaajabisha zaidi katika mechi zote 6 ambazo Yanga wameruhusu magoli magoli 6 yamefungwa kipindi cha kwanza, hapa pana ukakasi. Kwanini Yanga ishindwe kupata cleansheets mechi 6 kati ya 7?

Yanga ilifanikiwa kutokuruhusu bao mechi 7 kati ya 8 za mwanzo. Ukuta ule imara ulisimamiwa ipasavyo na Beno ukawanyima ruhusa yeyote Kagere Bocco na Okwi kuchungulia nyavu zao.

Leo hii timu dhaifu 5 zimefanikiwa kuchungulia nyavu za Yanga. Wana Yanga wanaweza kufurahia sana matokeo yao ya Come back lakini hebu tazama aina ya timu ambazo wamekuwa wakiwaruhusu mabao kabla ya wao kutoka nyuma



TAKWIMU YA TIMU AMBAZO ZIMEPATA GOLI DHIDI YA YANGA KATIKA MECHI 8 ZA MWISHO:

Tanzania Prisons: Wapo nafasi ya 19, wamefungwa mabao 19
Biashara: Wapo nafasi ya 20 wakiwa wameruhusu magoli 15
Mwadui: Wapo nafasi ya 15 na wameruhusu magoli 14
Ruvu: Wapo nafasi ya 16 na wameruhusu magoli 27 ( Tena hawa wamefanikiwa kupata magoli mawili)
Ndanda: Nafasi ya 14 na wamefungwa magoli 20.

Ukitizama kwa makini utagundua kuanzia nafasi ya 14 kushuka chini mpaka ya 20 timu zote zilizocheza dhidi ya Yanga zilizopo kwemye nafasi hizo wamepata bao lolote dhidi ya Yanga.

Kiufundi kuna tatizo ambalo Zahera anaweza aidha amelisababisha yeye kimfumo, au kukosekana kwa Beno, au kukosekana kwa umakini kwa mabeki wa Yanga au makosa binafsi ya walinda lango au makipa kushindwa kuwapanga vyema mabeki wake au pia kukosekana kwa Yondani kwaa baadhi ya mechi ingawa mchezo wa mwisho Yondani alikuwepo na Yanga waliruhusu bao.

Kagera Sugar pia imefanikiwa kuchungulia nyavu za Yanga. Wapo nafasi ya 9 lakini sio kwamba Kagera wana msimu mzuri sana la hasha. Kagera Sugar hawa hawa ilishindwa kupata bao dhidi ya Biashara, Lyon, Ruvu, Azam, Mtibwa na KMC lakini wakapata bao dhidi ya Yanga.

Msimu uliopita Yanga hawakuwa vizuri sana. Kulikuwepo na maelewano mabovu kiutendaji, kiwango hafifu cha Youthe Rostand goli, sekeseke la misharaha (Chirwa) lakini licha ya tafrani hizo Yanga katika mechi 16 za awali Yanga waliruhusu magoli 8 pekee huku msimu huu wakiruhusu magoli 11. Kuna nini?

Kuna mambo nadhani Zahera anaweza kurekebisha tu kirahisi. Mafunzo ya hali ya juu kwa Kabwili. Kabwili ni mdogo sana kumfokea Dante au Yondani. Najua tunamfahamu vyema Yondani sio rahisi hata kidogo kuongozwa na Kabwili lakini soka halina ukubwa au udogo. Matatizo kama haya yaliwahi kumtokea hata De gea alipojiunga na Man United. Alipata wakati mgumu sana kuwakoromea watu kama Vidic na Rio. Lakini baadae aliimarika kiasi chake.

Walinzi wa Yanga pia wanapaswa kuongeza umakini mkubwa sana ili kumuondolea Kabwili mzigo wa majukumu. Umri wa Yondani ni silaha tosha kuimarisha safu ya ulinzi. Kakolanya alikuwa sio muoga na hakujali jina au umri wa mtu. Mdogo wangu Kabwili yupo vizuri sana, kikubwa aendelee kuaminika naamini kesho nae ataziba pakacha la Yanga.

No comments:

Post a Comment