NI matumaini yangu muwazima na mko na hamu kubwa ya kujua kile ambacho nimewaandalia kwa siku ya leo. Kama kawaida sitatoka nje ya mapenzi. Nitazungumzia mapenzi kila siku kwa kuwa najua yanachukua sehemu kubwa sana katika maisha yetu ya kila siku. Mapenzi huweza kumfanya mtu akaishi maisha ya raha mustarehe hasa pale anapompata mtu mwenye penzi la kweli lakini pia usipoyajulia mapenzi yanaweza kukutoa roho.
Wangapi leo hii wamechanganyikiwa kutokana na kukataliwa penzi na watu waliotokea kuwapenda? Wangapi wamejiua baada ya kuachwa na wapenzi wao? Wangapi wanashindwa kufanya kazi zao kwa ufasaha kwa sababu wamekorofishwa na wapenzi wao? Hakika ni wengi na kwa maana hiyo basi kama unataka kuishi maisha ya raha, pamoja na mambo mengine hakikisha huchezi kamari kwenye mapenzi, ingia katika uhusiano unaofaa ili mwisho wa siku furaha ichukue nafasi katika kila siku iendayo kwa Mungu.
Wiki hii naomba nizungumzie swali ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza bila kupata majibu sahihi kiasi cha kuwafanya washindwe kuishi maisha ya furaha na wapenzi wao. ‘Hivi mpenzi wangu ananipenda kwa dhati?’ Hili ni swali wanalojiuliza wengi walio katika uhusiano.
Huenda hata wewe ulishawahi kujiuliza swali hili na mpaka sasa hujabaini ukweli wa penzi lake kwako na kama hujawahi kujiuliza swali hili basi hauko makini katika uhusiano wako. Hivi wewe ambaye unajiamini kwamba mpenzi wako anakupenda, kuna vigezo gani ambavyo vinakudhihirishia hilo? Labda niseme tu kwamba, mapenzi ya sasa yamejaa usanii wa hali ya juu sana. Unaweza ukajikuta uko na mpenzi ambaye anaonesha kukupenda, kukujali na kukuheshimu sana kiasi cha kukufanya uamini kwamba anakupenda kutoka moyoni mwake lakini kumbe anajifanyisha tu.
Yaani huo ndio ukweli wenyewe na usishangae hata huyo uliyenaye akawa anakupotezea muda wako tu. Unachotakiwa kukifanya ni kumfanyia uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa penzi lake kwako. Sawa huwezi kufunua moyo wake na kuangalia kama kweli anakupenda lakini kuna vitu vidogo vidogo vinavyoweza kukusaidia kumbaini mtu mwenye penzi la kilaghai.
JE, NI RAHISI KUMJUA?
Niseme tu kwamba hakuna mtu anayeweza kuwa na uhakika wa asilimia mia moja kuwa mpenzi wake anampenda kwa dhati na kama unaamini hivyo, unajidanganya. Hii ni siri ya mwenye kupenda na ndio maana unaweza kukuta mpenzi wako anakusisitizia kwamba anakupenda lakini bado unashindwa kuamini.
Wataalam wa masuala ya mapenzi wanasema, kumdhihirishia mpenzi wako kwamba unampenda sio lazima umwambie NAKUPENDA! Vitendo vyako ndivyo vitamfanya aamini hivyo. Penzi la kweli halifichiki Hukatazwi kumpenda mtu lakini bahati mbaya inakuwa pale utakapotokea kumpenda mtu asiyekupenda na akajilazimisha kukupenda ili kukuridhisha.
Walio katika aina hii ya mapenzi wako wengi. Mtu anaona kabisa mwanaume anamnyanyasa, anampiga, anamtukana, anamdhihaki, hamuoneshi kumpenda kwa dhati, hamjali lakini mwanamke anamng’ang’ania tu eti kwa sababu anampemnda sana. Hivi mwanamke kama huyu anashindwa kubaini kuwa mwanaume aliye naye hana penzi la dhati kwake?
Ifike wakati basi ukae chini na utafakari penzi analokupa mpenzi wako na kuchukua uamuzi sahihi, kumuacha au kuendelea naye. Usikubali hata siku moja kupotezewa wakati na mtu asiyelithamini penzi lako. Ni hayo tu kwa leo
No comments:
Post a Comment