MAPENZI ni hisia. Hisia kali za mapenzi zinaanzia moyoni. Macho yanaona, yanatamani, yanashawishika. Moyo unapokea matamanio na ushawishi wa macho. Hapo ndipo unaposikia mtu anakuambia, amempenda mtu kwelikweli kutoka moyoni. Bahati mbaya sana, moyo una sifa mno. Badala tu upokee matamanio na ushawishi wa macho, unahifadhi vitu hivyo viwili kwa pamoja. Halafu ukihifadhi, unageuka kuwa ruba. Unagandana nayo.
Hapo ndipo linapokuja suala la kumweka mtu moyoni. Moyo kaiwada yake ni king’ang’anizi. Unapenda matokeo chanya. Haukubaliani na matokeo hasi. Moyo unajiamini sana. Unaweza kupenda pasipopendeka, unaamini ipo siku tu utapendeka. Marafiki zangu, hapa ndipo tunaposhuhudia mateso mengi ya watu. Moyo unalazimisha kupenda. Unampenda mtu ambaye yawezekana akawa na mtu wake. Yawezekana akawa hana mtu, lakini hampendi tu.
Yawezekana unayelazimisha kumpenda naye ana sehemu anapenda, lakini hapendwi. Kila mmoja analia na moyo wake. Wewe unampenda huyu, hakupendi. Asiyekupenda naye anaye anayempenda, lakini huyo anayependwa naye hampendi. Moyo una kawaida ya kujipa matumaini. Kwamba si leo, labda kesho utapendwa. Unaulazimisha mwili, akili na macho ya mtu yaendelee kuishi na matumaini kwamba ipo siku nitakubaliwa. Yaani anaendelea kupambania penzi ambalo hajui lini litakaa sawa.
Ukweli upo hivi; unaweza ukalazimisha kupenda, lakini mwisho wa siku unayempenda si kwamba akawa hakupendi, lakini ana kipingamizi kinachomfanya asikukubalie. Anaweza kuwa na mtu wake ambaye naye anampenda kwa dhati au pengine naye hajakupenda, bila sababu yoyote.
Achana na mtu wa aina hiyo. Yupo mwingine ambaye aliingia kwenye uhusiano, akaamini kwamba yupo sehemu sahihi mwisho wa siku akaambulia mateso. Anaachwa solemba. Halafu akiachwa, hakubaliani na matokeo. Ubongo wake wake unapigwa upofu. Anashindwa kung’amua mambo. Akili yake haimfikirishi kurudi kwenye historia ya penzi lake. Je, lilikuwa na mizizi kiasi gani? Lilikuwa na malengo? Walikutana kwenye mazingira gani?
Fikra zake hazimpeleki kuwaza kwamba pengine alikuwa kwenye uhusiano na mtu ambaye ana mtu mwingine. Pengine yeye alikuwa wa zaida. Hawazi labda yawezekana aliyemuacha hakuwa na malengo naye zaidi ya kumchezea.
MUHIMU KUSEMA NA MOYO
Pamoja na kwamba moyo una kimbelembele cha kuhifadhi, jukumu la kupanga na kuchagua bado ni lako. Usikubali kupelekeshwa na moyo. Jitahidi kushindana nao japo wenyewe unajiona una nguvu kuliko akili na utashi wako. Uambie umechoshwa na masimango unayopewa. Unahitaji kuwa huru. Upumzike, umechoshwa na maneno makali yale ya kuambiwa ‘kwani huoni wengine hadi unipende mimi? Sikutaki, nimeshasema sikutaki!’
KUBALIANA NA MATOKEO
Moyo unapokuwa umependa huwa ni vigumu kukubaliana na matokeo ya kuachwa. Hautaki kukubaliana na jibu la kwamba; ‘nina mtu wangu, ninamheshimu.’ Lakini suala la msingi la kujiuliza, kwani moyo wako umefika kikomo cha kupenda?
Huwezi kumpenda mwingine zaidi ya huyo? Hata kama utaumia kwa muda fulani, lakini wahenga wana msemo usemao, kama ipoipo tu. Ipo siku utampata ambaye ndiye atakayekuwa wa kwako. Haijalishi utasubiri kiasi gani, lakini yupo tu mtakayeendana.
MTANGULIZE MUNGU
Kwa imani yako, amini Mungu ndiye muweza wa yote. Ndiye atakayekuletea mtu sahihi. Amini hilo ukimtumaini yeye hakuna kitakachoshindikana.
NIKUACHE NA SOMO HILI LA IMANI
“…mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradani mtauambia mlima huu, ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwepo neno lisilowezekana kwenu,” Matayo 17:20.
No comments:
Post a Comment